Arusha. Jiji la Arusha
limeteuliwa kuwa ni kati ya majiji 7,000 duniani kushiriki shindano la wasaa wa
mazingira linalolenga kupunguza athari za mabadiliko ya tabia nchini.
Kwa bara la Afrika, ni nchi
mbili tu, ambazo zipo katika mpango huo, ambazo ni Tanzania na Afrika Kusini.
Mradi huu, ambao hapa nchini
unaratibiwa na shirika la kimataifa la Mazingira (WWF), pia unalenga kupunguza
tatizo la ongezeko la hewa ya ukaa duniani.
Katika mradi huu, Jiji la
Arusha linapaswa kuongeza upandaji wa miti, kuongeza jitihada za usafi wa
mazingira na kuanza mipango ya matumizi ya nishati mbadala.
Ofisa Nishati Jadidifu wa WWF,
Philipina Shayo anasema Arusha ina fursa ya kubadilika kutokana na kuingizwa
katika mradi huu.
Shayo anasema katika mradi
huo, utakaofanyika katika nchi 18 duniani, miji ya Moshi na Dar es Salaam
itanufaika.
Anasema mradi huu ni wa mitatu
2014-2016 ambao lengo lake ni kuchangia katika kutoa elimu endelevu katika
matumizi ya nishati mbadala ili kupunguza tatizo la ongezeko la hewa ya ukaa na
mabadiliko ya tabia nchi.
Mratibu wa program ya nishati
jadidifu wa WWF, Dk Thelesia Olemako. Anasema Arusha ina bahati kubwa kuingizwa
katika mpango huu.
Licha ya kutambuliwa kidunia
katika vita dhidi ya athari za mabadiliko ya tabia nchi, pia itatajwa kuwa moja
ya majiji ambayo yapo katika mpango wa kupunguza hewa ya ukaa.
Meya wa Arusha, Gaudence Lymo
anasema jiji limejipanga kushiriki katika mradi huo, ili kukabiliana na
matatizo ya tabianchi na ongezeko la hewa ya ukaa.
Lyimo anasema katika mradi huo
wa Wasaa wa Mazingira, Jiji la Arusha, litajitahidi kuendelea kutunza mazingira
kwa kupanda miti, kufanya usafi na kutunza mazingira licha ya ongezeko kubwa la
watu kuwepo.
Naye mwenyekiti wa kamati ya
ya huduma za jamii, Isaya Doita anaeleza mipango ya jiji itafanikiwa katika
mradi huu.
Anasema hadi sasa miti zaidi
ya milioni 3 imezalishwa na miti zaidi ya 500,000 inaendelea kupandwa maeneo
mbalimbali ya jiji.
Hata hivyo anafafanua kuwa
kufanikiwa kwa mradi huu pia kunasukumwa na ushirikiano baina ya wananchi,
viongozi wa kisiasa na wakuu wa idara.
Ofisa wa afya wa jiji, James
Lobikoki anasema kukamilisha ujenzi wa jalala la kisasa, ujenzi uliogharimu
kiasi cha Sh4.3 milioni, ni nafasi ya kufanya vizuri katika mashindano haya.
Anasema dampo hilo, ambalo kwa
siku linapokea tani 385 za taka, linasaidia sana kupunguza tatizo la kusambaa
kwa taka mbalimbali katika jiji hilo.
Kauli za viongozi hawa wa jiji
na WWF zinapaswa kuwa ni faraja kwa jiji. Anasema hata kama Arusha haitashinda
kuwa kati ya majiji bora duniani, wananchi watanufaika.
Fursa hii inapaswa kutumika,
kusaidia jiji la Arusha kuboresha miradi ya mazingira ya upandaji miti,
uanzishwaji wa kiwanda cha kusaga taka na kutengeneza mkaa ili miti isikatwe na
pia kutumika dapo kuzalisha umeme.
Kuingizwa kwa Jiji la Arusha
katika mpango huu, pia kutasaidia kuanzishwa miradi ya umemejua sambamba na
matumizi ya vifaa visivyotumia umeme mkubwa. Hali kadhalika kutawezesha maeneo
ya pembezoni kusaidiwa miradi ya nishati jadidifu ili kuachana matumizi ya
nishati kubwa ya umeme.
Jiji la Arusha pia linapaswa
kusaidiwa kuwa na mradi kabambe wa kuhakikisha miradi ya kukusanya taka
inaimarishwa, mpango wa ukusanyaji maji taka unaboreshwa na pia kufukuliwa
mifereji ya asili ya majitaka.
Zamani, Arusha ilikuwa ni jiji
la baridi, mito ya maji safi, kama Naura na Ngarenaro, ilikatisha katikati ya
jiji, lakini sasa imegeuka maeneo ya kutupa taka na maji yamebaki ni historia.
Hivyo ni matumaini ya
wengi mradi wa wasaa wa mazingira, utalinufaisha Jiji la Arusha kurejea katika
uhalisia wake na hivyo kupungua kwa joto, na kuongezeka kwa mvua.
Chanzo cha Habari
~Mwananchi~
No comments:
Post a Comment