March 19, 2015

Dk Kilahama: ATHARI ZA MAZINGIRA SASA ZINAVURUGA UCHUMI NCHINI


Uharibifu wa misitu wa namna hii hufanywa na jamii  kwa ajili ya shughuli  za kilimo. 
Utafiti uliofanywa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kutumia mradi wake wa Tathmini ya Rasilimali za Misitu, 2013 unaonyesha kuwa tani milioni moja za mkaa kila mwaka hutokana na ukataji wa misitu.Hali hiyo inachagizwa na ukosefu wa ajira hususan katika maeneo yanayoathiriwa zaidi na shughuli hizo.Takwimu za uhifadhi wa mazingira zinaonyesha Tanzania hupoteza hekta 400,000 za misitu kila mwaka kupitia matumizi ya kuni, mkaa, mbao, ujenzi na uchomaji moto misitu.Nimefanya mahojiano na Mkurugenzi Mstaafu wa Idara ya Misitu na Nyuki, Dk Felician Kilahama ili kujua hatma ya taifa kwa miaka kadhaa ijayo.
Swali: Kwanza wananchi wangependa kujua hali ikoje kwa sasa katika ukataji wa misitu.
Jibu: Hali ilivyo siyo nzuri hata kidogo. Nathubutu kusema kuwa kiwango cha ukataji miti hasa katika misitu ya asili kiko juu na cha kutisha.Miti ya aina mbalimbali inakatwa kama haina mwenyewe kwa ajili ya kukata magogo ili kupata mbao za viwango mbalimbali, nguzo za kujengea nyumba, kuni, mkaa na mahitaji mengine mengi.
Swali: Ni maeneo gani ambayo unadhani yatakuwa yameathiriwa zaidi na uharibifu huo?
Jibu: Ukiachilia mbali mahitaji ya kawaida ya mbao, nishati na nguzo za kujengea, misitu inafyekwa kwa sababu ya kupata makazi mapya, kilimo na mifugo.
Katika baadhi ya mikoa kama Kigoma, Katavi, Morogoro, Rukwa, Ruvuma na Tabora maeneo mengi ya misitu yamevurugwa kutokana na makundi makubwa ya mifugo iliyohamishwa kutoka mikoa ya Arusha, Geita, Mwanza, Shinyanga, Manyara na Simiyu.
Swali: Tathmini yako kwa miaka 30 ijayo, Tanzania itakuwa kwenye hali gani licha ya kuwa na eneo kubwa la hifadhi ya misitu?
Jibu: Ni kweli Tanzania ilibahatika kuwa na maeneo ya misitu yaliyohifadhiwa kama 600 ya Serikali na 200 ya Halmashauri ya Wilaya.Misitu hiyo katika ujumla wake ni hekta zipatazo milioni 13. Misitu mingi ilihifadhiwa nyakati za ukoloni, miaka ya 1940 na 1950.Mwaka 1998 serikali za vijiji zimeweza kuhifadhi misitu ndani ya ardhi ya vijiji vyao. Hadi 2012 hekta zaidi ya milioni nne zilikuwa zimehifadhiwa kuwa ya hifadhi ya vijiji au jamii na kulifanya taifa liwe na zaidi ya hekta milioni 17.
Hali ni mbaya kama ilivyo kwa Pugu na Kazimzumbwi au Ruvu Kusini ambayo ipo karibu na Dar es Salaam lakini shughuli za kibinadamu zimekithiri kiasi cha kuifanya isiwe na uwezo wa kuhimili kazi zake za kiikolojia kama tunavyotakiwa kuiona ikifanya, ikiwa ni pamoja na kuhifadhia mazingira pamoja na kurutubisha, kuhifadhi udongo na kuboresha hali ya hewa.Uongo tuache, kwa miaka 30 ijayo iwapo kasi ya matumizi ya rasilimali za misitu itaendelea kuwa kama ilivyo bila kudhibitiwa, tusitegemee miujiza bali hali itakuwa mbaya zaidi na maisha kwa wengi kuwa magumu sana.Kitakachotokea, rasilimali maji itapungua sana, ukame kuwa wa kutisha na usalama wa chakula kuwa tatizo kubwa. Wanyamapori wataathirika sana kiasi cha kutishia shughuli za utalii na mapato ya taifa na wananchi kwa ujumla.
Swali: Nani ambaye anatakiwa kulaumiwa katika mazingira haya yanayoipeleka nchi kuwa jangwa?
Jibu: Serikali ni mwangalizi zaidi lakini mtengeneza jangwa ni mwananchi mwenyeji, yaani ni sisi watumiaji wa ardhi na rasilimali zilizo juu na ndani.
Hata hivyo, siasa imekuwa kinara cha kila kitu katika taifa letu. Kwa suala hilo, baadhi ya anasiasa wanaangalia zaidi masilahi yao binafsi kuliko uhai wa taifa.Turudi kwenye utawala wa sheria. Wanasiasa waheshimu hizo sheria wanazozitunga kwa faida ya nchi. Ukichunguza sana utaona siasa inachukua nafasi kubwa zaidi kuliko utaalamu.Mimi naamini wataalamu wakipewa nafasi yao na mawazo au ushauri wao ukazingatiwa kwa kiwango kikubwa tutaweza kusonga mbele katika kuliletea taifa maendeleo endelevu na kwa faida ya wengi.
Swali: Uzoefu wako, unadhani kuna athari gani ambazo zimeshaanza kuashiria matokeo ya uharibifu huo?
Jibu: Uwezo wa misitu yetu kama tungekuwa tunaisimamia vizuri, tungepata miti meta za ujazo kama 44 milioni.
Kwa bahati mbaya taifa linatumia karibu mita za ujazo 67 milioni ikiashiria kukata miti sana kuliko inavyotakiwa. Hii inamaanisha matumizi zaidi ya kiwango ya meta za ujazo zaidi ya 23 milioni.Kwa maneno mengine tunatumia miti ambayo ingetumika miaka 30 ijayo. Hiyo ni kuigeuza nchi jangwa.Maelezo ya Kilahama yanaashiria kuwa zinahitajika mbinu na mikakati bora ili kuliepusha taifa na hatari ambayo inaweza kutokea kwa sehemu kubwa ya nchi kugeuka jangwa. Badala ya wanasiasa kujijali zaidi yao au kuogopa kukemea tabia inayoathiri mazingira kwa woga wa kupoteza kura, wasimamie katika ukweli kwa faida ya Taifa na vizazi vijavyo.

No comments:

Post a Comment